top of page

Mkataba wa Bandari - TISS Imempiga Changa la Macho Rais?

Updated: Jul 14, 2023



Sakata la mkataba wa bandari linaendelea kukua kila kukicha. Wakati wananchi wengi wa kawaida, na viongozi vya vyama vya siasa nchini wakitoa kauli za kupinga mkataba huo, Chama Cha Mapinduzi kimeridhia kwa kauli moja kuendelezwa kwa makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali ya Tanzania na Dubai. Hii ni baada ya Bunge kuidhinisha makubaliano hayo mawiki kadhaa yaliyopita. Zaidi ya yote serikali kupitia kwa msemaji wake mkuu Bw. Gerson Msigwa imeeleza kuwa imedhamiria kusonga mbele na mpango huo licha ya kelele zinazoendelea. Kimsingi serikali ilishaamua, inatekeleza, haihitaji ushauri.


Kwa kifupi mjadala wa suala hili umesaidia sana kudhihirisha sura na mitazamo ya wananchi na viongozi wetu. Wapo wanaouunga mkono makubaliano hayo kwa kufuata mkumbo, bila kujua undani wa yaliyomo. Wapo pia wanaounga mkono kwa kuamini kwamba serikali huwa haikosei. Lolote itakaloamua liwe zuri au linaumiza ni sawa, na ni kwa faida ya watanzania. Halafu wako wale wanaounga mkono kwa sababu za uchawa. Hawa ni wale wasiojali faida wala hasara ya mkataba, wanachojali ni kujipendekeza kwa kiongozi wa nchi ili wapendwe na walau siku moja wafikiriwe kupewa teuzi.


Lakini wako pia watu wenye hekima zao, viongozi wastaafu waliojijengea heshima kubwa, na wanasheria waliobobea ambao wameonesha mashaka, na kutoridhishwa na mkataba huo. Hawa wameeleza kwa kina wasiwasi wao kuhusu makubaliano husika, kwamba hayafai. Yanaweza kututia katika matatizo makubwa ikiwa pamoja na migogoro ya kimataifa, ukoloni mambo leo, na umaskini wa kizazi na kizazi.


Wakongwe wa sheria kama kina profesa Shivji, mheshimiwa Tundulisu, Fatuma Karume, Dr. Slaa na wengine wengi wameonesha kutoridhishwa na mkataba huu, achilia mbali wana siasa nguli kama profesa Tibaijuka na mzee Butiku. Nao wana harakati maarufu na wenye kuheshimika kama Maria Sarungi wamefanya mikutano mingi kupitia mitandao ya kijamii (space) kujaribu kuishawishi serikali kutafakari upya suala hili bila mafanikio.


Kinachoonekana ni kuwa serikali imeamua kupuuzia kelele za wananchi bila hofu; Tena kwenye kipindi tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa rais na wabunge mwaka 2025. Hii ni serikali inayojiamini kwelikweli. Hakuna anayeweza kusema kwa uhakika kama kujiamini huko kunatokana na uhakika wa kushinda uchaguzi kwa kura au sababu nyinginezo.


Labda nikumbushe tu ile methali ya kiswahili isemayo 'Kilio cha wengi ni sauti ya Mungu.' Mwalimu Nyerere alijua maana ya methali hii, na hakuipuuza. Ndiyo maana hata baada ya 80% ya watanzania kuunga mkono mfumo wa chama kimoja, yeye akaona vyema Tanzania iingie mfumo wa vyama vingi vya siasa kukidhi haja ya wale 20% walioudai.


Mwalimu angeweza kutumia kigezo cha 'wengi wape' kukataa mabadiliko ya mfumo wa siasa, na hakuna mtu yeyote angemlaumu. Lakini alijua hoja za wale 20% zilikuwa nzito, na zilijaa ufahamu wa mambo yaliyokuwa yakiendelea duniani. Lilikuwa kundi la watu wenye weledi (informed), hivyo kuwanyima haki kungeweza kusababisha matatizo makubwa baadae. Mwalimu akatumia hekima kufanya maamuzi.


Halikadharika, ukiangalia kwa undani suala la makubaliano haya utaona kundi kubwa la watu wanaopiga kelele kupinga makubaliano haya ni wasomi, wanasheria nguli, wachumi, na viongozi wastaafu waliolitumikia taifa hili kwa uaminifu. Watu wanaojua sheria na taratibu za mikataba, na wenye wafuasi nyuma yao. Tena wana hoja nzito, zenye mantiki, na zinazoungwa mkono na historia ya bara la Afrika.


Hawa si aina ya watu wa kupuuza. Serikali ina kila sababu ya kuwasikiliza, tena kwa umakini mkubwa kabla ya mambo hayajaharibika. Viongozi wote hawa wanaunga mkono suala la uendelezaji bandari lakini hawakubaliani na aina ya mkataba tulioingia. Hili ni jambo ambalo serikali inapaswa kulitafakari na si kuwaandama watoa hoja.

Tuache hayo. Kama kuna chombo kilichopaswa kuwa cha kwanza kupinga wazo la kuwapa DP World bandari zetu (kama ilivyoainishwa kwenye IGA) ni idara ya usalama wa Taifa (TISS). Bila shaka idara ilijua mpango huu tangu likiwa wazo la mtu mmoja tu. Yaani kabla hata mazungumzo ya awali kuanza. Idara ilipaswa kuchunguza kwa kina, kusasambua, na kufanya tathmini ya ndani kuhusu faida na hasara zitakazojitokeza endapo Tanzania itaingia makubaliano hayo, na kupendekeze aina ya makubaliano yenye maslahi kwa nchi.


Si hivyo tu bali pia idara ilipaswa kuangalia kwa makini hatua kwa hatua taratibu za uandaaji na utiaji sahihi makubaliano hayo, kuhakikisha viongozi/wataalam wetu hawanunuliwi, hawasukumwi na tamaa ya mali, hawatishiwi, wala kushawishiwa kwa namna yoyote ile kukubali kipengele chochote chenye utata, au kinachoelekea kuitia hasara nchi yetu kuingizwa kwenye mkataba.


Kwa kifupi hata wabunge waliopelekwa Dubai kwenda kujifunza toka kwa DP walipaswa kuangaliwa kwa makini. Kuchunguzwa kama walipewa rushwa, au waliahidiwa zawadi ili kuwashawishi wabunge wengine kupitisha makubaliano/mkataba husika. Kwa kawaida idara ilipaswa kupenyeza maafisa wake katika msafara huo, na bila shaka ilifanya hivyo.


Mwingine anaweza kujiuliza "idara inahusikaje kwenye suala la mikataba ya biashara kati ya nchi yetu na nchi nyingine?" Kwa kifupi idara ndiyo yenye dhamana ya kuhakikisha nchi yetu haifanyiwi hujuma ya aina yoyote ile. Idara inapaswa kuhakikisha nchi za kigeni hazitumii makampuni binafsi au mawakala wa serikali zao kujipenyeza nchini kwetu kwa lengo la kufanya vitendo vya kiadui, na au kuweka misingi ya kulisambaratisha Taifa letu ki uchumi, kisiasa na kijamii.


Huu ni wajibu usiohitaji maelekezo wala mjadala wa ziada. Idara ina nguvu na uwezo wa kutumia wanasheria na wataalam wa ndani na nje ya idara kwa kadri inavyoona inafaa kwa maslahi na usalama wa Taifa. Tena inao maafisa vipenyo katika pembe zote wanaolipwa kwa kufanya majukumu mazito kwa faida na usalama wa Taifa.


Wakati wa mwalimu Nyerere, kiongozi mmoja alipewa nafasi ya kwenda Hungary kununua mabasi ya kampuni ya UDA. Kiongozi huyo alifanya kazi nzuri sana. Alifanikisha mpango wa kuleta mabasi makubwa yaliyoungana kama gari moshi maarufu kwa jina la ICARUS 'kumbakumba.' Mabasi haya yalisaidia sana kupunguza msongamano wa abiria jijini Dar es Salaam.


Pamoja na kazi nzuri aliyofanya mzee huyo, idara ilibaini kwamba kampuni ya ICARUS ilimzawadia mzee huyo basi moja dogo, kama ahsante ya kusaini mkataba huo (Ten percent). Mambo yakawa si mambo. Kwa kifupi kiongozi huyo alinyang'anywa basi alilopewa, na akafukuzwa kazi. Tena kwa kusemwa vibaya kama bedui au bepari aliyeitia hasara nchi. Wakati mzee wa watu hata hilo basi hakudai apewe, kilikuwa kiherehere cha wazungu tu.


Hebu fikiria hiyo ilikuwa zawadi ya basi moja tu, tena aliyopewa baada ya kufanikisha mkataba mzuri kwa taifa. Hakuuza Roliondo wala kugawa sehemu ya ardhi ya Tanzania kwa mtu. Huyo alikuwa mwalimu Nyerere, kiongozi aliyeheshimu kanuni na maadili ya uongozi. Leo hii iko wapi idara ile yenye weledi na maono ya kuilinda na kuitetea Tanzania?


Ukitafakari sakata la mkataba huu mambo mawili yanaweza kukujia kichwani. Jambo la kwanza, ni kwamba idara haikufanya kazi yake ipasavyo. Iliwaamini mawaziri, makatibu wakuu wa wizara, na wataalam wengine wa mambo ya bandari, na kuwaacha wafanye kazi yao kwa uhuru.


Kama hili ndilo lililotokea, basi idara imefanya kosa kubwa mno! Tena inastahili kulaumiwa kwa kuiingiza nchi kwenye mgogoro. Ni wajibu wa idara kuhakikisha Tanzania haifanywi shamba la bibi, wala nchi za kigeni hazifanyi mipango ya muda mrefu kutaka kuiingiza nchi yetu kwenye utumwa wa kiuchumi, ukoloni mamboleo, au migogoro ya kimataifa. Ilikuwa na bado inao wajibu wa kuwadhibiti viongozi hawa.



Jambo la pili ni kuwa idara ilifanya kazi yake vizuri na kumshauri mheshimiwa rais kama ilivyopaswa. Lakini kwa mamlaka aliyokuwanayo, mheshimiwa rais akaamua kutupilia mbali ushauri huo, na kufuata ushauri wa wataalam wengine. Hili si jambo la ajabu. Hata Rais wa Marekani enzi hizo Donard Trump kuna wakati aligoma kusikiliza ushauri wa vyombo vyake vya usalama. Hata hivyo, matokeo yake leo hii kila mtu anayajua.


Kwa ujumla ni jambo la kutia shaka mno rais wa nchi anapoacha kuisikiliza idara yake ya usalama, na kutegemea ushauri toka sehemu nyingine kwa mambo makubwa ya kiusalama. Ni hatari inayoweza kumdumbukiza shimoni. Hili liliwahi kutokea Tanzania huko nyuma enzi za kina Alhaj Kitwana Kondo na Profesa Kighoma Malima. Wanaokumbuka enzi hizo wanajua nini kilitokea.


Ni dhahiri huwa kuna sababu zinazoweza kumfanya kiongozi wa nchi aipuuze idara yake. Sababu kubwa zaidi huwa udhaifu wa ushauri unaotolewa na idara kulinganisha na ubora wa ushauri unaopatikana toka kwa watu wengine walio karibu na rais. Tatizo kiongozi akijizoeza utaratibu huu anaweza kujikuta akishauriwa na Andre Cohen (Master spy).


Kwa vile mkurugenzi mkuu wa TISS aliyepo madarakani hivi sasa (DGIS) Bw. Said Hussein Nassoro ameteuliwa hivi karibuni, ni vigumu kujua kama ndiye aliyehusika na ushauri huo au mtangulizi wake Bw. Diwani Msuya ndiye anayestahili kubeba lawama. Hata hivyo kama DGIS aliyepo sasa hakuhusika, na hapendezwi na makubaliano hayo bila shaka mambo yangekuwa tofauti na yalivyo sasa.


Upo pia uwezekano kwamba idara ilifanya kazi yake juu juu na kumpa rais taarifa isiyo na uchambuzi wa kina. Makosa ya aina hii huweza kutokea endapo maafisa waliopewa kazi ya kufuatilia, kufanya uchambuzi, au kuandika taarifa ya kumpa rais hawana ujuzi sahihi katika fani husika. Maafisa wa idara huitwa 'jack of all trades' kwa sababu ya uwezo wao wa kujua na kufanya mambo mengi. Hii hufanya mara nyingine waaminiwe kutoa ushauri hata katika masuala yanayohitaji mtaalamu mahususi.


Idara inatambua hilo, ndiyo maana imejitahidi kuajiri wasomi wa kila fani katika vitengo vyake. Wapo wachumi, wanadiplomasia, wanasheria, wataalam wa sayansi ya siasa n.k. Wasiwasi uliopo ni kuwa idara ina mapungufu ya wataalam wa uchambuzi na watabiri wa muelekeo wa hali ya nchi na dunia nzima kiusalama, kisiasa, kiuchumi na kijamii. Hili linajidhihirisha katika mfumo mzima wa uongozi na utendaji wa mihimili ya serikali yetu, na yanapotokea matatizo kama hili la makubaliano ya uwekezaji bandari.

Inawezekana idara imeridhika kwa kuwa na maafisa wengi wenye shahada mbili au tatu na hivyo kuamini ina wasomi wa kutosha, na kupuuzia umahili wa kuwa na wachambuzi mahili wa fani husika kiitelijensia. Tatizo hili linaweza kuonekana kama dogo, lakini linaifanya idara idharaulike, au ushauri wake usiwe na nguvu ya ushawishi kwani hauna tofauti na ule unaotolewa na wataalam wengine, wasio maafisa wa idara.


Pengine ni kwa sababu hii watu wanaotumiwa na serikali kuelimisha wananchi juu ya uzuri wa uendelezaji bandari zetu wanang'ang'ana kuzungumzia uwezo wa DP katika uendeshaji, badala ya kuzungumzia aina ya makubaliano yaliyofanyika, na athari zake kwa uchumi na dola ya Tanzania kwa vizazi vijavyo. Ni kama kutetea hoja ya kumpa mtu shamba la ngano kwa kisingizio cha ufundi wake wa kupika mikate.


Kwa ujumla nguvu ya idara iko katika kuona mambo ambayo wataalam wengine hawawezi kuyaona, na kutoa ushauri uliosheheni kweli ambazo wengine hawawezi kuzijua. Nguvu hii huimarishwa kwa ukusanyaji wa taarifa sahihi, uchambuzi wa kitaalam, na uwasilishaji (ushauri) sahihi. Idara ni macho na masikio ya serikali. Idara inaposhindwa kuona na kusikia ni wazi serikali itakuwa kipofu. Kwa bahati mbaya kipofu siku zote huwa katika hatari ya kudumbukia shimoni. Nachelea makubaliano haya yasije yakawa shimo lingine!


Ustawi wa Tanzania - Jukumu letu sote.

Rev. Godwin Chilewa




130 views0 comments
bottom of page